Tuesday, April 14, 2020
NEWS: WAZIRI MKUU ATOA MAAMUZI MAPYA JUU YA UGONJWA
Waziri Mkuu amesema agizo la kufungwa kwa shule za awali, Msingi, Sekondari na Vyuo vyote vya elimu ya kati na vya elimu ya juu litaendelea kubaki vile vile hadi hapo Serikali itakapotoa tamko jingine. Pia, Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. John Pombe Magufuli amesitisha maadhimisho ya Sherehe za Mapinduzi (Aprili 26) pamoja na Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei Mosi) ili kuepuka msongamano na kuendelea kuzuia virusi vya corona visisambae zaidi. Waziri Mkuu ameyasema hayo leo katika kikao cha Kamati ya Kitaifa ya Uratibu wa Mapambano Dhidi ya ugonjwa wa Homa ya Mapafu unaotokana na maambukizi ya Virusi vya Corona Amesema hadi leo, nchini kuna jumla ya watu 53 waliobainika kuwa na virusi vya corona ikiwa ni ongezeko la wagonjwa wanne ambao wote wapo jijini Dar es Salaam. Amesema Serikali bado haijatangaza kuhusu kufunguliwa kwa shule, vyuo na shughuli za michezo pamoja na misongamano isiyokuwa ya lazima, hivyo maeneo hayo yataendelea kusalia katika karantini na wanafunzi wote wandelee kubakia majumbani kwao. Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli ameagiza sh. milioni 500 ambazo zilitengwa kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 56 ya Sherehe za Muungano zipelekwe kwenye mfuko wa kupambana na COVID-19 wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Pia, Waziri Mkuu amewaomba wadau mbalimbali waendelee kuiunga mkono Serikali katika mapambano dhidi ya virusi vya corona kwani janga hilo ni kubwa na wanaweza kutuma fedha kupitia akaunti Na: 9921159801 yenye jina la National Relief Fund Electronic. Kadhalika, Waziri Mkuu amesema elimu ya tahadhari ni muhimu ikaendelea kutolewa kwa wananchi ili waweze kujikinga na maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona. “Kama si lazima kutoka, wananchi waendelee kutulia majumbani mwao.”
Tags
NEWS
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment